KIONGOZI WA KIROHO
Kiongozi
wa kiroho ni tofauti na kiongozi asiye wa kiroho kwa kuwa kiongozi wa
kiroho ni mtumishi anayewatumikia anaowaongoza wakati huyu kiongozi
mwingine hutumikiwa na wale anaowaongoza. Yesu ni mfano kamili wa
kiongozi wa kiroho.
- (Marko 10:45) Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
- (Yohana 13:4-5) aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga
- (Marko 10:43) Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu. Na kwahiyo sifa kuu ya kiongozi wa kiroho ni kuwa mnyenyekevu na kuwa na huruma.
- (Luka 7:12-13) Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.
Mzee wa
kanisa ili atimize vyema wajibu wake ni lazima pia aijue taasisi
anayoitwa kuiongoza. Kanisa ni mali ya Mungu aliyoinunua kwa damu ya
mwanae Yesu Kristo na kuiweka chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu ili
itumike hapa duniani kama chombo cha wokovu kwa wanadamu wote. (Matendo
ya Mitume 20:28) Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo
Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate
kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.
Kanisa
ndicho kitu cha thamani sana hapa duniani kwani kilinunuliwa kwa damu ya
thamani ya Yesu. (Matendo ya Mitume 20:28) Jitunzeni nafsi zenu, na
lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa
waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. (Waefeso 5:25) Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake.
Ingawa shetani kwa karne nyingi amejaribu kuliharibu kanisa hili, Yesu
ameendelea kutimiza ahadi yake ya kulilinda na nguvu za kuzimu.(Mathayo
16:18) Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Mwamba unaotajwa hapa si Petro bali ni Yesu mwenyewe. (1 Wakorintho
10:4) Wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea
mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Yeye
ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema
naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea
maneno ya uzima atupe sisi. (Matendo ya Mitume 7:38). Kristo ndiye
kichwa cha kanisa. (Waefeso 5:23) Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe,
kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Mzee wa
kanisa asiruhusu watu kugeuza kanisa kuwa mahali pa kupimania ubavu,
ubabe na kutambiana juu ya nani aliye bora kuliko mwingine. Wala
asiruhusu kanisa kugawika kwa misingi ya watu wenye ushawishi au ukabila
kwa kuwa si Paulo wala Kefa aliyelinunua hili kanisa. (1 Wakorintho
1:12, 13) Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema,
Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni
wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili
yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?
Yesu
alikuja duniani kuondoa ukuta uliokuwa umetugawa sisi tuliokuwa
wamataifa na Wayahudi. (Waefeso 3:6) Ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja
nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa
ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Ukuta huo
aliubomoa kwa kutoa kafara ya upatanisho iliyotuwezesha sisi tuliokuwa
wamataifa pamoja na wale waliokuwa warithi wa ahadi za kimwili
zilizotolewa kwa Abrahamu kuhesabiwa haki ya kuwa warithi wa Agano
Jipya. Yesu anawathamini wale walioko nje ya zizi hili kama
anavyotuthamini sisi. Yeye huwaita wale walio kwenye zizi lile ni kondoo
wake. (Yohana 10:16) Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na
hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako
kundi moja na mchungaji mmoja (Wagalatia 3:27-28). Hili hututangazia
kuwa sisi tulio kanisani hatupaswi kujigawa makundi makundi ya
kubaguana. Kuta hizo Yesu alikwisha kuzivunja. (Wagalatia 3:27 – 29)
Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana
Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu
mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Moja ya wajibu
mkubwa wa kanisa leo ni kuifanya hekima hii ijulikane kwa ulimwengu
wote.
Kuitwa
kuwa mzee wa kanisa ni kupewa heshima kubwa kwa kuwa anayestahili
heshima hiyo ni Yesu mwenyewe. Wazee wa kanisa ndiyo viongozi wa kwanza
kabisa kuwekwa ili kulilinda na kulichunga kanisa lake Mungu. (Matendo
ya Mitume 14:23) Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa,
na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana
waliyemwamini. Paulo alikutana nao wazee hawa mara kwa mara na kuwapa
maelekezo muhimu ya usimamizi wa kanisa la Mungu kama tufanyavyo leo.
(Matendo ya Mitume 20:17) Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso,
akawaita wazee wa kanisa. Hawa ndiyo waifanyao kazi pamoja na Kristo
kulisafisha kanisa lake ili lisiwe na kunyanzi. (Waefeso 5:27) Apate
kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama
hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.
SIFA YA MZEE WA KANISA
Sifa za wazee zimetajwa katika Agano la Kale na Agano jipya kwa mafungu yafuatayo:
“Zaidi
ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha
Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu
yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na
wakuu wa kumi.” (Kutoka 18:21)
“Ni
neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi
imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na
busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa
kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana,
wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema,
ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia
nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu
aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.
Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika
lawama na mtego wa Ibilisi.” 1 Timotheo 3:1-7
MAJUKUMU YA MZEE WA KANISA
Majukumu
ya Mzee wa Kanisa yamegawanyika katika Nyanja tatu: Kuchunga,
Kusimamia, na Kuongoza (kuwa kielelezo au kuonesha njia). (1 Petro
5:1-4) Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na
shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa
baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia,
si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka
fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya
mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.
KUCHUNGA:
Mtu
huchungwa kwa kuhakikisha amekula chakula anachokihitaji na kwa kiasi
atakachoshiba. Utafiti unaonesha kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya
watu waasi na kuacha kutembea na watu wa Mungu, ni mafundisho potofu
wanayopewa na waasi wenzao. Ili kuzuia ongezeko hilo mzee wa kanisa
atahakikisha washiriki wake anawapatia mafundisho ya misingi ishirini na
nane kwa ukamilifu na kuchukua muda wa kujibu hoja za kisera
zinazotolewa na waenezao mafundisho ya uongo. Kuchunga pia kutahusisha
kutembelea washiriki majumbani na kutembelea kwenye makundi mara kwa
mara akiyaimarisha ili yaweze kukua na kuwa kanisa. Kuhubiri kila Sabato
na kuhakikisha waliopangwa kwa mahubiri wanakidhi hitaji. Kuhakikisha
watu walio kwenye eneo lake wanafikiwa na injili ya Yesu na hivyo
kuongeza idadi ya washiriki wake kila mwaka angalao kwa 25% ya washiriki
waliopo. Kuona kuwa washiriki wananunua Biblia, Miongozo ya kujifunza
Biblia na kitabu cha Tumaini Kuu kwa ajili yao wenyewe na kwa kugawia
wasiofikiwa na injili yetu. Kuona kuwa kila idara inajihusisha na
shughuli za uinjilisti. Kuona kuwa jengo la ibada linaboreshwa ili
lifanane na heshima ya Mungu tunayemwabudu.
KUSIMAMIA:
Mchungaji
asipokuwepo mzee wa kanisa atasimamia baraza la Kanisa na kushughulikia
kujaza nafasi zilizo wazi, kutoa adhabu kwa waumini, kwa kadri
atakavyoelekezwa na mchungaji, ataendesha meza ya Bwana, atatoa
matangazo, atatoa semina kwa watenda kazi, atapitisha wanaohama na
wanaohamia, ataendesha huduma ya mazishi, atahudhuria semina,
atakaribisha wageni na kuwaandalia huduma za malazi na chakula, atatuma
taarifa kunakohusika, atakuwa msemaji wa kanisa. Atasimamia ratiba za
vipindi na kuona kuwa wahusika wanazingatia muda uliopangwa na ya kwamba
vipindi vinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo na maelekezo yaliyopo.
Kuhakikisha kanisa lina dira na mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu
unaofafanua namna mtakavyofikia viwango vya juu vya ukuaji katika siku
za usoni. Wazee watumie madaraka waliyopewa kukemea wale wenye mazoea ya
kulisumbua kanisa na kuyumbisha washiriki ikiwa baada ya kupewa semina
bado wameendelea kukaza shingo. (1 Timotheo 5:20) Wale wadumuo kutenda
dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.
KUONGOZA:
Mchungaji
ataongoza kwa kuonesha kielelezo kwa mwonekano, vitendo, na kauli.
Ataonyesha uongozi wa utumishi kwa kuwavuta anaowaongoza na kamwe
hatafanya kazi kwa kulazimisha au kwa manung’uniko. Atafungua milango
kwa washiriki ili wamfikie kwa matatizo yao, atashauri na kusuluhisha
migogoro, atakuwa mwaminifu na mwadilifu, ataimarisha umoja na kupiga
vita ubaguzi wa namna yoyote. Atawahimiza na kuwatia shime washiriki
wake kutumia fursa zilizopo na uwezo walio nao kujiletea maendeleo ya
kiuchumi, kiakili, kijamii, na kiroho na hivyo kuboresha maisha yao nay a
kanisa. Atawahimiza kutimiza wajibu wao kwa lugha ya kiungwana na staha
huku akiwaelekeza kwa Kristo
MIPAKA YA MZEE WA KANISA
Wazee
wa kanisa watawekeana zamu ili kutoa fursa kwa asiye zamu kushiriki
huduma za makundini au huduma zingine. Mzee kiongozi ndiye atakayehusika
kuendesha vikao vya baraza la Kanisa mchungaji asipokuwepo, pamoja na
matangazo, lakini anaweza kukasimu madaraka hayo kwa wengine akitaka.
Kila idara itapewa mzee mmoja atakayeisimamia kwenye vikao vyake na
kuihimiza itekeleze majuku yake. Mzee wa kanisa ni mzee hadi kundini
hivyo ataweka kwenye ratiba yake siku za kutembelea kundini kwa semina
na kusalimu washiriki. Mzee wa kanisa hatahudumu katika kanisa amabalo
halijamchagua isipokuwa kwa kibali cha mchungaji wa mtaa. Kipindi cha
mzee kukaa madarakani ni mwaka mmoja au miwili kutegemeana na maamuzi
yaliyopitishwa na mashauri ya kanisa. Ikiwa baada ya muda huo mzee
ataonekana bado anahitajika katika utumishi wake, na ikiwa watu wengine
wenye sifa kama ya kwake hawapatikani, kanisa linaweza kumchagua tena.
WASAIDIZI WA MZEE WA KANISA
Mzee wa
kanisa atatakiwa awape uzoefu na kuwapa shime watendaji walio chini
yake akiwaelekeza namna ya kufanya kazi zao kwa ufanisi. Asiwalaumu
wanapokosea bali awaonye kwa unyenyekevu akiwakumbuka kwenye maombi yake
ili roho awasaidie kubadilika. Mzee awashirikishe wenzake katika
maamuzi wala asipende kufanya maamuzi peke yake. Awathamini watendaji
wenzake akitambua kuwa kazi inayofanywa kwa ushirikiano kama timu ndiyo
inayofaulu. Mara kwa mara awapongeze na kuwashukuru wale wanaofanya vema
ili wapate nguvu ya kuendelea kufanya vizuri. Asiruhusu wasaidizi wake
kuchukua nafasi yake kwa kuwa mambo yatakapoharibika ni yeye
atakayewajibika. Akubali kuwajibika kwa makosa ya wasaidizi wake.
MIIKO YA MZEE WA KANISA:
Ni
mwiko kwa mzee wa kanisa kutoa siri za Baraza au za washiriki
anaowatembelea kwa watu wasiohusika. Ni mwiko pia kwa mzee kutembelea
washiriki akiandamana na mtenda kazi wa jinsia tofauti na kuwa na
ukaribu unaokaribisha maswali na mashaka. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa
kutumia fedha za kanisa bila idhini ya baraza la kanisa. Ni mwiko kwa
mzee wa kanisa kumsimamisha kazi au kumpa adhabu mshiriki bila idhini ya
baraza la kanisa na mashauri ya kanisa. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa
kumzuia mchungaji wa mtaa wake kuhudumu kwenye kanisa au kundi alilopo.
Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kugomea maagizo yaliyotoka ngazi za juu kwa
utashi wake mwenyewe au kwa kushinikizwa na kanisa lake. Ni mwiko kwa
mzee wa kanisa kuruhusu kikundi chochote cha kanisa kutoka nje ya kanisa
lake au kikundi cha kanisa lanje kutembelea kanisa lake bila taarifa na
idhini ya mchungaji. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kuruhusu kutumia
mimbari watu waliokatazwa na uongozi wa juu kutumika kanisani. Ni mwiko
kwa mzee wa kanisa kutompokea na kumwandalia malazi na chakula mgeni wa
kanisa aliyewatembelea. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kugomesha kanisa
kutokuja mkutanoni au kwenye makambi kwa sababu yoyote ile.
WAJIBU WA WASHIRIKI KWA MZEE WA KANISA
Mzee wa
kanisa anafanya kazi nyingi za kanisa kwa kutumia muda wake na wakati
mwingine kwa kutumia mali zake na hivyo kanisa linapaswa kuonesha
kutambua ukweli huo kwa kumpa heshima anayostahili. (1 Petro 2:17-18)
Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima
mfalme. Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa hofu nyingi, sio wao
walio wema na wenye upole tu, bali nao walio wakali. Tena mahali pengine
mtumishi wa Mungu amesisitiza akisema. (Waebrania 13:17) Watiini wenye
kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho
zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha
wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.