2 Bwana Yesu Kristo Asifiwe! Jambo la 2 la kufanya ikiwa hali yako ya maombi si nzuri, na
unashindwa kumwomba Mungu inavyotakiwa: Ondoa hali ya kujihukumu moyoni mwako! Kujihukumu moyoni mwako kunakuondolea ujasiri wa kwenda mbele za Mungu na kuomba. Biblia inasema hivi: "Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake...."(1Yohana 3:21,22). Huu ni mstari unamhusu yule anayeshindwa kuomba, au kwa sababu anadhani ya kuwa hata baada ya kutubu Mungu hajamsamehe! Au ameshindwa kujisamehe kwa sababu ya kosa alilomkosea Mungu, hata kama amelitubia kosa hilo! Au anajisikia vibaya moyoni, akidhani ya kuwa, kwa kuwa wale wanaomzunguka hawaonyeshi hali ya kumsamehe kwa kosa alilofanya, basi anafikiri na Mungu naye hajamsamehe hata kama ametubu! Amini ya kuwa Mungu hasemi uongo! Ukitubu dhambi zako huwa anakusamehe na kuifuta dhambi hiyo! Hii ni sawa na Isaya 1:18 na Isaya 43:25 na 1Yohana 1:9. Mungu anasema hivi kwako:"Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie maana nimekukomboa"(Isaya 44:22). 3 Jina la Yesu Kristo liedelee kutukuzwa milele! Jambo la 3 la kufanya ikiwa hali yako ya maombi si nzuri, na unashindwa kumwomba Mungu inavyotakiwa: "Funga katika nafsi yako"! Hebu soma mstari huu: "Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; maombi yangu yakarejea kifuani mwangu"(Zaburi 35:13). Daudi aliyasema hayo alipokuwa anatafuta utatuzi wa yeye kushindwa kuomba kama alivyokuwa anaomba huko nyuma! Daudi anasema kufunga katika nafsi yake, kulisaidia kurejesha tena maombi kifuani mwake! Na wewe wewe unaweza ukatumia mbinu kama hii, ili kurudisha tena uwezo wako wa kuomba! Fahamu ya kuwa: kuna tofauti kati ya kufunga katika mwili, na kule kufunga katika nafsi. Kufunga katika mwili maana yake, kuunyima mwili mahitaji yake muhimu kama chakula; na maji na usingizi. Kufunga katika nafsi maania yake,kuinyima nafsi yako mahitaji yake muhimu yanayopatikana kwa njia ya macho na masikio. Lakini ikiwa ni kufunga katika mwili au ni katika nafsi; ni muhimu uongozwe na Roho Mtakatifu sawasawa na neno la biblia. Kwa hiyo, kufunga katika nafsi kunatokea mtu anapofanya maamuzi ya makusudi kwa msukumo wa Roho Mtakatifu moyoni mwake, ili kujitenga na kukaa kwa utulivu mahali ambapo hakuna usumbufu juu ya macho yake na masikio yake. Ukifanya hivi, tarajia maombi kurudi kifuani mwako sawa na Zaburi 35:15. Tunakuombea ili Mungu azidi kukufundisha na kukuongoza katika kufanya maombi ya kufunga yenye faida