Mnamo 8-14/5/2011 kulifanyika Rally kubwa sana ya
Vijana iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Vijana wa Tanzania Union Mchungaji
Joseph Dzo’mbe. Rally ilisheheni
mada za kutosha zikiwemo semina za Vijana na Utandawazi, Uamsho na
Matengezo katika Idara ya Vijana, Ifahamu Idara ya Vijana, Malezi ya
Watoto, Mwongozo wa kujifunza Biblia katika Shule ya Sabato (angalia
somo lililo tolewa). Pia kulikuwa na Mahubiri yaliyogusa mioyo ya wajumbe walio hudhuria.
Aidha,
Rally hii ni maandalizi ya Kambi kubwa linalo tegemewa kufanyika October
27 – November 5, 2011 ambalo litafanyika katika shamba la Kibidula. Kambi
hili limekusudiwa kuwa na wanakambi wasiopungua 2500 kutoka katika
makanisa yote ya Conference ya Southern Highlands yanayo kadiriwa kuwa
250. Hivyo lengo kwa kila kanisa ni kuleta wanakambi wasiopungua 10. Huo
ni wastani wa chini
Mkurugenzi wa Vijana Tanzania Union akitoa Semina ya Mwongozo wa Kujifunza Biblia Wakati wa Shule ya Sabato.
KUJIFUNZA MWONGOZO WA BIBLIA (BIBLE STUDY GUIDE)
Kuna walimu wa aina mbili wa Mwongozo wa Biblia katika Shule ya Sabato.
- Walimu wanaofundisha Mwongozo wa Biblia (Lesson) baada ya kupitia kozi maalum inayotolewa na GC kwa muda wa miaka mitatu. Cheti hutolewa kwa wahitimu wa kozi hii kinachowatambulisha kuwa walimu wa mwongozo wa Biblia wa Shule ya Sabato.
- Walimu wanaofundisha kozi hii baada ya kupitia kozi ya masaa 10. Kozi hii ni ufupisho wa kozi ya miaka mitatu. Kozi hii huendeshwa kwa ushirikiano kati ya idara ya vijana ya Shule ya Sabato.
MALENGO YA IDARA YA SHULE YA SABATO
Idara ya Shule ya Sabato ina malengo makuu matatu.
- Kuwafundisha washiriki kuzielewa kweli za Biblia.
- Kuhimiza huduma ya utume ulimwenguni kwa njia ya sadaka.
- Kuhimiza ushirika wa kikristo na umoja miongoni mwa waumini.
SABABU ZA KUFUNDISHA MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA
Wako watu wengine wanaosema kuwa hakuna haja ya kuwa na mwongozo wa kujifunza Biblia maana Roho Mtakatifu anatosha.
Biblia na Roho ya
Unabii vinaikataa dhana hii. Wanafunzi wa Yesu walifundishwa miaka
mitatu na nusu. Hata baada ya Yesu kupaa kwenda mbinguni waliendelea
kujifunza. Tutaendelea kujifunza habari za wokovu wetu mpaka mwisho wa wakati.
UMUHIMU WA KUWA NA DARASA LA WALIMU
- Huwasaidia walimu kutoka na mawazo yanayofanana katika kuwafundisha wana darasa.
- Hupanua mawazo ya walimu na kuondoa utata miongoni mwao.
- Huwajenga na kuwakuza walimu kiroho.
- Hukuza moyo wa umoja na mshikamano miongoni mwa walimu.
- Hukuza karama ya ufundishaji kwa walimu.
- Huwafanya kuwa wataalamu wa maandiko. Kadiri wanavyofundisha wao hubakiwa na maarifa zaidi.
VITENDEA KAZI IVYA MWALIMU WA MWONGOZO WA BIBLIA WA SHULE YA SABATO
- Biblia
- Mwongozo wa kujifunza Biblia toleo la mwalimu
- Vitabu vya rejea kama vilivyoainishwa kwenye mwongozo.
- Notebook na kalamu.
UFUNDISHAJI WA DARASA LA WALIMU
Darasa la walimu huendeshwa siku ya Sabato asubuhi au muda mwingine kwa kadiri ya makubaliano ya walimu. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kufundisha darasa la walimu.
- Ijue barabara ya somo. Ili kujua barabara ya somo, oanisha kichwa cha somo, fungu la kukariri, utangulizi na hitimisho siku ya Ijumaa.
- Toa muhtasari wa somo kwa kufuata mtiriko wa somo kama ulivyoanishwa toka mwanzo wa somo hadi mwisho. Mtiririko huo uhusishe maswali makuu yaliyoko katika mwongozo wa mwalimu ambayo hukamilisha lengo la mtunzi wa somo.
- Waruhusu walimu wa darasa kuchangia somo na kuboresha barabara halisi ya somo.
- Walimu walihusianishe somo na maisha ya kila siku. (Life application)
- Walimu wajadili utata wowote uliojitokeza katika somo.
- Msimamizi wa darasa akumbuke kukaza maarifa kwa kutaja mambo makuu ya msingi ambayo wana darasa wanapaswa kuyafamu. Walimu wa madarasa watamkumbusha ikiwa kuna mambo mengine ya muhimu ya kwenda kukazia kwa wana darasa.
NAMNA YA KUFUNDISHA DARASA LA WATU 6 -8
Mwalimu wa darasa
anapaswa kutambua kuwa yeye ni mwalimu na pia ni msimamizi wa darasa. Ni
mwalimu kwa kuwa atawaelekeza wana darasa katika barabara ya somo na
mwishoni mwa kipindi ndiye atakaye kazia yale mambo muhimu katika somo
kama yalivyoainishwa na darasa la walimu. Ni msimamizi kwa kuwa atawasimamia wana darasa katika kujadili somo na kuhakikisha kuwa wana darasa hawatoki nje ya somo. Mambo yafuatayo yafanyike katika darasa.
- Kusalimiana na kutambulishana hasa kama kuna wageni.
- Kupata taarifa za wasiohudhuria na kupanga utaratibu wa kuwatembelea.
- Kutoa taarifa ya kushuhudia kulikofanywa na wana darasa katikati ya wiki. Wana darasa wasitoe shukrani jinsi Mungu alivyowalinda, bali waeleze jinsi walivyomfanyia Bwana wao kazi.
- Kiongozi wa darasa aeleze utaratibu wa kushuhudia wiki ijayo, na kuwatia moyo wana darasa kuja na taarifa za kumfanyia Bwana wao kazi.
- Kupiga magoti wawili na kuombea kikosi chao, mipango iliyojadiliwa, kuombea wasiokuwepo na kuombea somo la leo.
KUINGIA KWENYE SOMO
- Wafundishe wana darasa wako utangulizi wa somo kwa kuhusianisha kichwa cha somo, fungu la kukariri, utangulizi na hitimisho. Kwa kufanya hivyo utakuwa umewaweka wana darasa katika barabara ya somo.
- Waruhusu wana darasa kuchangia sehemu yoyote ya somo wanayojisikia kufanya hivyo. Wakati huo huo wasaidie wana darasa wasitoke nje ya barabara ya somo.
- Waelekeze wana darasa kulifananisha somo na maisha yetu ya kila siku.
- Waruhusu kuuliza maswali ikiwa kuna mahali hapajaeleweka, na waruhusu wana darasa kumjibu mwenzao. Ikiwa hajaridhika mwalimu aweza kumwongezea. Ikiwa muda haukutosha kutosheleza majibu katika swali hilo, au ikiwa swali hili litahitaji jibu la muda mrefu, mwaweza kupanga kukutana wakati mwingine kushughulikia jambo hilo.
- Kabla ya kumaliza somo, kumbuka kukazia mambo makuu wana darasa wanayopaswa kutoka nayo katika somo hilo.
VIPENGELE VYA KUANGALIA UNAPOFUNDISHA NA KUSIMAMIA SOMO
- Fundisha mtu na wala sio darasa. Waelewe watu wako. Waulize maswali rahisi wale wasiopenda kuongea. Kila mtu ashirikishwe kwa namna moja au nyingine katika kuchangia somo.
- Simamia darasa kwa uchangamfu na tabasamu.
- Waite wana darasa kwa majina.
- Elewa muda wa kuanza somo na muda wa kumaliza somo.
- Uwe nadhifu. Sehemu zozote zinazohitaji kufungwa, kama vile vifungo na zipu ziwe zimefungwa.
- Wakumbushe wana darasa kuzima simu kwenye ibada.
- Heshimu mawazo ya kila mwana darasa.
- Watazame wana darasa usoni unaposema jambo.
- Tumia lugha rahisi.
- Toa sauti ya kusikika.
- Shirikisha viungo vya mwili katika kufundisha somo.
- Kama darasa lina watu pungufu ya 8 keti unapofundisha.
- Epuka kuhubiri. Wape nafasi ya kutosha wana darasa kuchangia somo.
Washiriki wakisikiliza kwa makini mahubiri wakati wa mkutano wa Rally huko Mlowo – Mbozi